Utawala wa Rais wa Marekani, Joe Biden unajaribu kupunguza hali yoyote ya sintofahamu inayoweza kutokea kwa China kutokana na ziara ijayo ya Rais wa Taiwan, Tsai Ing-wen nchini Marekani.
Rais Tsai atasimama California na New York baadaye mwezi huu kabla ya kuanza safari rasmi ya Amerika ya Kati.
Afisa wa utawala ambaye hakutajwa jina anasema utawala wa rais Biden umeiambia Beijing kwamba marais wa zamani wa Taiwan walifanya ziara za mara kwa mara nchini Marekani wakielekea mataifa mengine, ikiwa ni pamoja na Tsai, ambaye amefanya ziara sita kati ya 2016 na 2019.
Afisa huyo anasema China haipaswi kutumia kusimama kwa Tsai nchini Marekani kama sababu ya kuchukua hatua yoyote kali dhidi ya Taiwan.