Marekani yaishinikiza Hamas kukubali pendekezo la sitisho la mapigano kwa wiki sita

  • VOA News

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Cameron wakifanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Washington, Aprili 9, 2024.

Marekani Jumanne ililishinikiza kundi la Hamas kukubali makubaliano ya kusitisha mapigano na Israel huko Gaza kwa muda wa wiki sita, na pia kuachiliwa huru kwa mateka 100 wanaoshikiliwa na kundi hilo, ili Israel nayo iwaachilie huru mamia ya Wapalestina iliowafunga jela.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken aliwambia waandishi wa habari mjini Washington kwamba “ni pendekezo “muhimu sana” lililowasilishwa kwa Hamas mjini Cairo mwishoni mwa Juma lililopita na lazima likubaliwe.”

“Kazi sasa ni kwa Hamas,” Blinken alisema.

“Ulimwengu unasubiri kuona kile Hamas itafanya.”

Israel ilitangaza vita dhidi ya Hamas baada ya shambulio baya la kigaidi la Oktoba 7 ndani ya Israel, ambalo liliua watu 1,200 na kupelekea watu 250 kushikwa mateka.

Mashambulizi ya Israel yaliyofuatia tukio hilo yameua zaidi ya watu 33,000 huko Gaza, karibu theluthi mbili wakiwa wanawake na watoto, kulingana na maafisa wa afya wa Gaza, huku jeshi la Israel likisema maelfu kadhaa ya wapiganaji wa Hamas ni miongoni mwa waliouawa.

Kufikia katikati mwa mwezi Februari, mateka 112 waliachiwa huru, wengi wao wakati wa sitisho la mapigano la wiki nzima mwezi Novemba, huku wengine zaidi ya 36 wakihofiwa wamekufa au waliuawa huko Gaza katika kipindi cha miezi sita ya mapigano.