Marekani yafanya shambulizi jingine la anga Somalia

Wanamgambo wa Al Shabab wakifanya mazoezi kwenye picha ya maktaba

Marekani Jumapili imethibitisha kufanya shambulizi la tatu la anga dhidi ya wanamgambo wa al-Shabab ndani ya kipindi cha chini ya wiki mbili nchini Somalia.

Shambulizi la Jumapili linasemekana llitekelezwa ili kuvisaidia vikosi vya serikali ya Somalia katika ujirani wa Geycad kwenye jimbo la kati la Galmudug, kulingana na ripoti ya jeshi.

Serikali ya Somalia awali iliripoti shambulizi lilikuwa katika eneo ambako majeshi ya serikali kuu na yale yaliyopatiwa mafunzo na Marekani yalikuwa yakipambana na wanamgambo. Hakuna ripoti zozote iwapo wanamgambo walijeruhiwa au kuuawa.

"Hili ni pigo jingine kubwa kwa al-Shabab ikimaanisha katika vita vyao dhidi ya watu wa Somalia," taarifa ya wizara ya habari ya Somalia imesema.

Wote Marekani na serikali ya Somalia hawajasema endapo kulikuwa na maafa kwa raia.

Al-Shabab hata hivyo, imesema katika taarifa yake iliyochapishwa katika mtandao kwamba majeshi ya serikali, yaliyokuwa yanasaidiwa na Marekani, hayakufanikiwa katika mapigano ya Jumapili.

mashambulizi ya awali ya anga yalifanyika Julai 20 na 23 katika eneo hilo hilo. Haya ni mashambulizi ya kwanza dhidi ya al-Shabab nchini Somalia tangu Rais wa Marekani Joe Biden achukue madaraka mwezi Januari.