Makomando wa Somalia, walioshambuliwa na kundi la kigaidi la al-Shabab, kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miezi kadhaa, wamepata usaidizi kutoka Marekani kupitia shambulizi la anga, jana Jumanne.
Pentagon imethibitisha kwamba majeshi ya Marekani, yalifanya shambulizi moja karibu na mji wa Galkayo, takriban kilomita 580, kaskazini mwa mji mkuu wa Mogadishu, ambalo lilitangazwa kwa mara ya kwanza, na maafisa wa serikali ya Somalia mapema hapo jana.
Afisa wa Pentagon, ameiambia VOA kwamba shambulizi hilo, liliidhinishwa chini ya mamlaka zilizopo, kulinda vikosi vya washirika wa Marekani, na lilifanyika, hata ingawa hakuna wanajeshi wa Marekani, waliokuwa kwenye ardhi ya Somalia. Shambulizi hilo, lililolenga wanamgambo wa Al-shabaab, ni la kwanza, ndani ya kipindi cha miezi sita, na la kwanza kutekelezwa, tangu Rais wa Marekani, Joe Biden, aingie madarakani.