Marekani yafanya mashambulizi ya kulipiza kisasi nchini Iraq na Syria

Ramani ya Iraq

Marekani Ijumaa ilifanya mashambulizi ya anga huko Mashariki ya Kati kulipiza kisasi baada ya shambulio baya la ndege isiyokuwa na rubani kwenye kambi ya wanajeshi wa Marekani nchini Jordan Jumapili iliyopita lililoua wanajeshi watatu wa Marekani.

Kamandi kuu ya jeshi la Marekani ilisema wanajeshi wake walifanya mashambulizi ya anga ndani ya Iraq na Syria dhidi ya kikosi cha mapinduzi cha Iran, Iran’s Islamic Revolutionary Guards Corps (IRGC) na makundi ya wanamgambo yenye uhusiano na kikosi hicho.

Jeshi la Marekani lilishambulia zaidi ya malengo 85 kwa kutumia ndege kadhaa.

“Tulishambulia mahali tulipokusudia kushambulia,” alisema Luteni Jenerali Douglas Sims, ambaye anahudumu kama mkuu wa operesheni kwa niaba ya wakuu wa jeshi la pamoja la Marekani.

Alisema shambulio hilo la anga lilifanyika kwa takriban dakika 30 na kwamba maeneo matatu kati ya maeneo yaliyoshambuliwa yalikuwa nchini Iraq na manne yalikuwa Syria.

Maafisa wa Marekani wamesema Iraq ilifahamishwa kabla ya shambulio hilo kutekelezwa.

Rais wa Marekani Joe Biden alisema mashambulizi hayo yalitekelezwa kutokana na amri yake.

“Jibu letu limeanza leo. Mashambulizi yataendelea kwa muda na wapi tutaamua yaelekezwe. Marekani haitaki mzozo Mashariki ya Kati au katika eneo lolote duniani lakini kwa wale wote wanaotaka kutuhujumu waelewe haya: Ukimuhujumu Mmarekani, tutajibu,” alisema Biden katika taarifa jana Ijumaa.