Huku akikiri kuongezeka kwa wasiwasi kuelekea vita kamili kati ya Israel na Hezbollah, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, amesema, hakuna upande hata mmoja unaotaka vita.
Amesema haamini Hezbollah inataka vita, ameiambia hadhira katika taasisi yenye makao yake mjini Washington ya Brookings. Amesema pia Israel haitaki vita, ingawa wanaweza kuwa tayari kukabiliana na vita endapo italazimika kufanya hivyo.
Ameongeza kusema kwamba Lebanon haitaki vita kwa sababu itakuwa mwathirika mkuu wa vita hivyo, na Iran pia haitaki vita kwa kiasi fulani kwa sababu inataka kuhakikisha Hezbollah haitokomezwi na inaweza kuishikilia Hezbollah kama turufu endapo itaihitaji.
Maoni ya Blinken yametolewa wakati Israeli ikiashiria shinikizo la chini la kijeshi Gaza litaruhusu vikosi vyake kutenga rasilimali zaidi kushughulikia tishio linaloletwa na Hezbollah inayoungwa mkono na Iran upande wa kaskazini.
Blinken alirudia wito wake kwa kiongozi wa Hamas wa Gaza, Yahya Sinwar, kukubali pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano na kusema Washington imedhamiria kutoachwa nyuma katika ujenzi mpya wa Gaza baada ya vita.