Marekani Jumanne imesema itatoa kiasi cha hadi dola milioni 10 kwa atakaetoa habari kuhusu watu 6 wanaotambulishwa kama maafisa wa ujasusi wa jeshi la Russia, ambao waliendesha mashambulizi ya mtandaoni yaliyoathiri miundombinu muhimu ya Marekani.
Maafisa hao wanafanya kazi katika kitengo cha idara kuu ya ujasusi ya Russia kinachohusika na masuala ya mtandaoni ( GRU) ambao walihusika katika shambulio la mwaka wa 2017 kwenye ngazi ya kimataifa la kusambaza kirusi kilichoharibu kompyuta za makampuni kadhaa ya kibinafsi ya Marekani, ikiwemo mfumo wa hospitali, wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema.
Shambulio hilo la mtandaoni maarufu “NotPetya” la 2017 lilidumaza sehemu ya miundombinu ya Ukraine na kuharibu kompyuta katika nchi kote ulimwenguni, ikiwemo Ufaransa, Ujerumani, Italy na Marekani, na kusababisha hasara inayokadiriwa kuwa ya mabilioni ya dola.
Russia ilikanusha kuhusika katika shambulio hilo.