Jopo la wajumbe hukaa na kumchagua rais atakayeliongoza taifa la Marekani. Jopo hilo huwa na wanachama 538. Idadi ya wajumbe inatofautiana kati ya jimbo na jimbo kutegemea na idadi ya wapiga kura. Kwa majimbo yenye idadi ndogo ya wapiga huwa na wajumbe wachache na yale yenye idadi kubwa huwa na wajumbe wengi zaidi.
Mgombea ambaye anapata wingi wa kura za wajumbe ndiyo anakuwa mshindi wa nafasi ya urais. Ili mgombea urais kuweza kutangazwa mshindi anatakiwa awe amepata wingi wa kura 270.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa George Kakoti wa chuo kikuu cha Nova South Eastern huko Florida anasema wajumbe wa jopo hili maarufu kama Electoral College wanachaguliwa kulingana na mfumo uliowekwa katika kila jimbo.
Your browser doesn’t support HTML5
Kila baada ya miaka minne wapiga wa Marekani huchagua rais na makamu rais na mgombea ambaye anashinda wingi wa kura katika kila jimbo isipokuwa mawili tu ndiyo hupata kura zote za jopo la wajumbe. Majimbo mawili ambayo hayafuati mfumo wa mshindi anachukua wajumbe wote ni Nebraska na Maine ambapo kura zinagawiwa kulingana mfumo uliowekewa katika majimbo hayo.
Upigaji kura unapokamilika, kwa mfano katika uchaguzi wa mwaka huu itakuwa ni Novemba 8, hivyo mwezi unaofuata wajumbe wa jopo hukutana na kumchagua rais, wajumbe hawa si wabunge au maseneta, bali ni maafisa waliochaguliwa katika majimbo, viongozi wa vyama, au watu wenye mshikamano wa karibu na wagombea urais.
Wanakutana mwezi mmoja baada ya upigaji kura na hapo ndipo hupiga kura zao, profesa Kakoti anasema wajumbe hawa hawawajibiki kisheria wamchague mtu Fulani kushika wadhifa wa urais, wanaweza kufika na wakabadili msimamo wao na kumchagua mtu ambaye pengine jimbo lake halikupendekeza hivyo.
Ni vyema ikumbukwe kuwa wajumbe hawa watakutana katika wiki ya pili ya mwezi Desemba kupiga kura zao kumchagua rais, na kwa mwaka huu upigaji kura utakuwa Desemba 19 na baada ya hapo bunge litakutana Januari 6 mwakani kuhesabu kura hizo.