Marekani: Mwendesha mashtaka maalum ateuliwa kuchunguza nyaraka zilizopatikana kwenye ofisi ya zamani ya Rais Biden

Mwanasheria mkuu Merrick Garland akitangaza mbele ya waandishi wa habari, uteuzi wa mwendesha mashtaka maalum atakaechunguza nyaraka muhimu zilizopatikana kwenye ofisi ya zamani ya Rais Biden, Januari 12, 2023

Mwanasheria mkuu wa Marekani Merrick Garland Alhamisi alimteua mwendesha mashtaka maalum kuchunguza jinsi nyaraka muhimu ziliishia kuhifadhiwa kwenye ofisi ya zamani ya Rais Joe Biden mjini Washington na nyumbani kwake Wilmington, Delaware.

Garland alimchagua mwendesha mashtaka mwenye uzoefu Robert Hur, ambaye ni mwendesha mashtaka mkuu wa zamani katika jimbo la Maryland, kuendesha uchunguzi huo.

Hur alihudumu pia kama afisa mkuu kwenye wizara ya sheria wakati wa utawala wa Donald Trump.

Uamuzi wa Garland unafuatia uteuzi wake wa awali wa mwendesha mashtaka maalum Jack Smith kuendesha uchunguzi kama huo dhidi ya Trump. Kwa miezi kadhaa, rais huyo wa zamani alikataa kurudisha nyaraka muhimu za serikali kwenye idara ya kitaifa ya kuhifadhi nyaraka nyeti za serikali kama inavyoaagizwa na sheria ya Marekani, alipoondoka madarakani miaka miwili iliyopita na kuzipeleka nyaraka hizo kwenye makazi yake huko Florida.

Garland aliwambia waandishi wa habari kwamba uteuzi wa Hur unabaini nia ya dhati ya wizara ya sheria kwa ajili ya uhuru na uwajibikaji hasa kuhusu masuala nyeti.