Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema kwamba kuna uhakika kwamba Rwanda inawasaidia waasi wa kundi la M23 na kwamba waasi hao wametekeleza ukandamizaji mkubwa wa haki za kibinadamu.
“Tunasisitiza msimamo wetu kwamba ni lazima Rwanda iache kutoa msaada wa aina yoyote kwa kundi la M23 na kuondoa wanajeshi wake mashariki mwa DRC,” inasema ripoti hiyo ambayo imechapishwa kwenye wavuti wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani.
https://www.state.gov/statement-on-report-by-un-group-of-experts/
Taarifa ya Marekani inajiri siku chache baada ya kutolewa kwa ripoti ya wataalam wa umoja wa mataifa iliyotolewa Desemba 30, inayosema kwamba serikali ya Rwanda inawaunga mkono waasi mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Ripoti ya wataalam wa umoja wa mataifa inasema kwamba wamekusanya ushahidi wa kutosha kwamba “wanajeshi wa Rwnada wanahusika katika vita vya DRC moja kwa moja” na kwamba walishiriki katika mashambulizi yaliyotokea kati ya Novemba 2021 na Oktoba 2022.
“Wanajeshi wa Rwanda walianzisha oparesheni ya kuwapa nguvu waasi wa M23 kushambulia waasi kutoka kabila la wahutu la Democratic forces of liberation of Rwanda FDLR. Rwanda iliwapa silaha na sare za kijeshi waasi wa M23.” Inasema ripoti ya wataalam wa umoja wa mataifa.
Rwanda imekanusha madai ya kuunga mkono M23
Serikali ya Rwanda imekuwa ikikanusha ripoti kwamba inaunga mkono kundi la waasi la M23 na badala yake imesema kwamba serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo inaunga mkono waasi wa FDLR waliohusika na mauaji ya kimbari yam waka 1994.
Serikali ya Rwanda inachukuliwa kundi la FDLR kuwa tishio kubwa kwa usalama wa utawala wa rais Paul Kagame.
Kagame aliambia raia wa Rwanda katika hotuba yam waka mpya kwamba serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo “imeshindwa kuongoza sehemu za mashariki mwa DRC”
“Hali hii inaendelea kwa sababu DRC haipo tayari kuongoza sehemu yake. Rwanda haitakubali kubeba mzigo wa DRC,” alisema rais Kagame.
Ripoti ya wataalam wa umoja wa mataifa inasema kwamba hali ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo inaendelea kuharibika kabisa, saw ana hali ya kibinadamu.
Inataka viongozi wa jumuiya ya Afrika mashariki, Angola na nchi za maziwa makuu kuharakisha utekelezaji wa mikakati ya kumaliza vita mashariki mwa DRC.
“Tunatarajia kundi la M23 ambalo liliwekewa vikwazo na umoja wa mataifa kuondoka kulingana na makubaliano ya Angola, na tunaambia makundi yote yenye silaha, wakiwemo M23 kuacha vita, kuweka chini silaha na kuunga mkono mchakato wa amani wa Nairobi kati ya serikali ya DRC na makundi ya waasi.”
Ushirikiano kati ya jeshila DRC na FDLR
Marekani vile vile inataka jeshi la DRC kuacha kushirikiana na kundi la FDLR, namna ilivyofichuliwa katika ripoti ya wataalam wa umoja wa mataifa.
Mapigano yamepungua japo kuwa hali ya wasiwasi kati ya raia kuhusu usalama wao.
Kundi la M23 limeondoka katika baadhi ya sehemu lilikuwa linashikilia.
Sehemu hizo ni Kibumba, Rumagambo na Kishishe.
Jeshi la Jumuiya ya Afrika mashariki limeshika doria katika sehemu hizo baada ya kuondoka kwa waasi wa M23.
Wanajeshi wa jumuiya wameshika doria katika sehemu za Rumagambo, Kisigari na Rugari, kaskazini mwa mkoa wa Kivu.