Marekani kukata misaada kwa wanaopinga Jerusalem

Balozi Nikki Haley

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema nchi yake itakata misaada kwa nchi ambazo zinaliunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa la kupinga Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel.

Trump alitangaza kuitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel mapema mwezi huu na nchi wanachama wa jumuiya ya kimataifa kupinga hatua yake hiyo.

Trump alisema ''Tunawapa mamilioni na mabilioni ya dola kisha wanatupinga. Acha watupinge tutaokoa pesa nyingi. Hatujali.''

Matamshi hayo yanakuja ikiwa ni muda mfupi kabla ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kupiga kura kupinga kutambulika huko kwa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel, ambako kulitangazwa na Trump.

Mapema, muwakilishi wa Marekani Umoja wa Mataifa Nikki Haley waliwaonya mataifa ya umoja huo kuwa Trump amemtuma kupeleka majina ya nchi ambazo zimeipinga Marekani.

Haley amesema baada ya kura ya Jumatatu ya Baraza la Usalama, “ Marekani haitoambiwa nan chi yoyote mahali gani tuweke ubalozi wetu.” Ameonya nchi nyingine katika barua iliyoonyeshwa kwa VOA ikieleza kauli ile ile ya Trump.

Huko Umoja wa Mataifa, mabalozi kadhaa wamesema kuwa walipokea barua ya Haley, lakini hawajapanga kubadilisha msimamo wao.

“Msimamo wetu juu ya suala hili uko wazi, tumepata fursa ya kujieleza katika Baraza la Usalama, na huo ndiyo msimamo wetu thabiti,” amesema balozi wa Sweden katika UN, Olof Skoog. “Kwetu sisi hili siyo kabisa suala la mahusiano yetu na Marekani, ambao ni mzuri sana.”

Alhamisi Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa dharura uliombwa na mwakilishi wa Palestina Riyad Mansour ufanyike, na kuungwa mkono na nchi za Kiarabu na nchi zisizokuwa na mfungamano. Mansour amesema ni matarajio yake kuwa hatua hiyo itaungwa mkono na walio wengi.