Marekani kufanya kikao na Russia Januari

Rais wa Russia Vladimir Putin akifanya mkutano wa kimitandao na mwenzake wa Marekani Joe Biden kwenye picha ya awali.

Ikulu ya Marekani Alhamisi imesema Washington inaiangalia Moscow kwa ukaribu, na itazingatia masuala ya kidiplomasia kwenye mazungumzo yajayo ya kiwango cha juu.

Hili linatokea wakati kiongozi wa Russia, Alhamisi akishutumu Marekani na washirika wa NATO kwa kupuuza taifa lake wakati akiendelea kuongeza vikosi katika mpaka wa Russia na Ukraine.

Rais Vladimir Putin katika mkutano na wanahabari ameshutumu idara za kijasusi za mataifa ya magharibi kwa kujaribu kuvunja shirikisho la Russia kwa kutumia makundi ya kigaidi, na kuongeza operesheni za NATO upande wa mashariki.

Akijibu maswali ya wanahabari kuhusiana na shutuma za rais Putin, msemaji wa White House, Jen Psaki, Alhamisi amesema kwamba ni taarifa zinazoweka mambo hadharani kwamba Russia ndiyo inaongeza vikosi vyake katika mpaka wake na Ukraine pamoja na kuendeleza maneno. Psaki amesema Marekani itafanya mazungumzo ya ngazi ya juu na Russia mapema mwakani.