Maseneta wa Marekani wanaoitembelea Afrika Kusini kutathmini mafanikio ya mpango mkubwa wa kupambana na ukimwi unaofadhiliwa na Marekani, Alhamisi wameapa kuundeleza mpango huo licha ya uhusiano wa karibu wa Pretoria na Russia.
Afrika Kusini iliendelea na mazoezi ya pamoja ya majeshi ya majini yenye utata na Russia na China, yakifanyika sambamba na kumbukumbu ya mwaka mmoja ya uvamizi wa Kremlin dhidi ya Ukraine.
Mazoezi hayo yalizunduliwa Jumatano katika pwani ya mashariki mwa Afrika Kusini licha ya wito wa kuyaahirisha au kuyasitisha kabisa.
“Mnafanya mazoezi ya pamoja ya wanamaji na Russia na China wakati wa kumbukumbu ya mwaka mmoja ya uvamizi wa Vladimir Putin dhidi ya Ukraine, mtapata matatizo,” Seneta Mrepublican Lindsey Graham aliuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Johannesburg.
Pamoja na hayo, ameahidi kuwa ufadhili wa mpango huo wa kupambana na ukimwi utaidhinishwa tena.