Marekani yawatahadharisha raia wake Tanzania juu ya Ebola

Mfano wa kirusi kinachosababisha ugonjwa wa Ebola

Wizara ya Mambo ya Nje Marekani imesema Ijumaa katika ukurasa wake unaotoa taarifa za ushauri wa safari kwamba wasafiri wa Marekani wanatakiwa kuwa makini zaidi ikielezea ripoti ya kifo kinachoonekana kuhusiana na Ebola jijini Dar Es Salaam

Marekani inawaonya raia wake kuchukua tahadhari zaidi wakati wanapotembelea nchini Tanzania kufuatia wasi wasi juu ya ugonjwa wa Ebola na kuongeza kutoa wito kwa nchi hiyo kutoa taarifa kuhusu kesi zilizoshukiwa za ugonjwa wa Ebola.

Shirika la habari la Reuters linaripoti kuwa wizara ya mambo ya nje Marekani ilisema Ijumaa katika ukurasa wake unaotoa taarifa za ushauri wa safari kwamba wasafiri wa Marekani wanatakiwa kuwa makini zaidi ikielezea ripoti ya kifo kinachoonekana kuhusiana na Ebola jijini Dar Es Salaam.

Mfano wa kirusi cha ugonjwa wa Ebola.

Tanzania inakanusha ripoti hiyo ikisema hakuna kesi ya ugonjwa wa Ebola iliyothibitishwa nchini humo lakini kwa kuweka uwazi zaidi katika kupambana na ugonjwa huo unaosambaa haraka na kusababisha kifo, serikali ipo katika shinikizo la kutoa maelezo zaidi.

Wizara ya mambo ya nje Tanzania haikupatikana Jumamosi kujibu tahadhari iliyotolewa na Marekani. Maafisa katika nchi za mashariki na kati huko Afrika wamekuwepo kwenye angalizo la juu la uwezekano wa kusambaa kwa Ebola kutoka nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC mahala ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita mlipuko huo umeuwa zaidi ya watu 2,100.

Tanzania na DRC zinashirikiana mpaka ambao unatenganishwa na ziwa. Katika ukosoaji wa nadra kwa umma, shirika la afya Duniani-WHO wiki iliyopita lilieleza kwamba katika kupingana na kanuni za kimataifa za afya, Tanzania ilikataa kutoa taarifa za kina za kesi zinazoshukiwa kuwa za Ebola.