Marekani inatofautiana kupunguza wanajeshi wake Afrika

Kikosi maalumu cha jeshi la Marekani huko Niger

Waatalamu wa kijeshi wa Marekani wanatofautiana juu ya mipango ya awali ya kupunguza idadi ya operesheni maalum za jeshi la Marekani barani Afrika.

Gazeti la New York Times liliripoti kwanza juu ya mpango huo mapema mwezi June ikieleza kwamba kupunguzwa operesheni maalum kutaweza kupunguza idadi ya makomando wanaofanya kazi katika bara hilo kutoka 1,200 hadi kufikia 700 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Maafisa wa kijeshi wameiambia Sauti ya Amerika-VOA kwamba ingawa maafisa wa Pentagon wamekubaliana na sababu za msingi za kupunguza wanajeshi hao lakini hakuna uwamuzi wa mwisho uliochukuliwa.

Katika taarifa kwa VOA, Meja Sheryil Klinkel msemaji wa Pentagon alisema Marekani utathmini mara kwa mara jinsi inavyowatumia wanajeshi wake kote duniani na kufanya marekebisho kulingana na mahitaji yake.

Ndege ya kikosi maalumu cha jeshi la Marekani ikitua Nigeria

Pendekezo hilo linafuatia tathmini ya Pentagon ya tukio lililofanyika mwezi Oktoba 2017 ambapo wanajeshi maalum wa Kofia Ya Kijani wa Marekani walishambuliwa kwa kushtukiza na kuuliwa walipokua wanafanya doria nchini Niger.

Wachunguzi wa Pentango waligundua kuwepo na kasoro kadhaa, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mafunzo ya kutosha na usimamizi.

Balozi wa zamani wa Marekani huko Nigeria, John Campbell, ambaye ni mjumbe wa Baraza la Ushirikiao wa Kigeni alisema maafisa wa kijeshi wana wasiwasi kwamba wanajeshi maalum wanatumiwa kupita kiasi.

Lakini wengine wanahoji muda na sababu za kuchukuliwa uwamuzi huo kamanda wa zamani wa operesheni maalum kwa Afrika, Donald Bolduc alisema vitisho vilivyojitokeza katika shambulio la Niger ni ushahidi kwamba Marekani inahitaji kuendelea kuwepo katika kanda hiyo.

Hatua hii inatokea wakati China na Russia zinaongeza shughuli zao za kijeshi barani Afrika.