Makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano hayakutekelezwa lakini waziri Blinken alitangaza “Kufuatia mazungumzo katika muda wa saa 48 zilizopita, jeshi la Sudan na wanamgambo wa kikosi cha Rapid Support Forces( RSF) wamekubali kutekeleza sitisho la mapigano nchi nzima kuanzia usiku wa manane tarehe 24 Aprili, litakalodumu saa 72.”
Taarifa ya Blinken imetolewa saa mbili kabla ya makubaliano hayo kuanza kutekelezwa.
Mapigano hayo ni kati ya wanajeshi watiifu kwa mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na wale wa makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Dagalo, ambaye ni kamanda wa kikosi cha RSF.
Takriban watu 427 wameuawa na zaidi ya 3.700 kujeruhiwa, kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa mataifa.
Miongoni mwa waliouawa hivi karibuni ni afisa kwenye ubalozi wa Misri mjini Khartoum. Wizara ya mambo ya nje ya Misri imethibitisha kifo cha afisa huyo, ambaye aliuawa akielekea ubalozini kutoka nyumbani kwake kupewa maelekezo ya utaratibu wa kuondoka nchini Sudan.