Marekani imetoa vikwazo zaidi dhidi ya mitandao ya kibiashara inayowalenga wa-Houthi na Hezbollah, wizara ya fedha ya Marekani imesema, wakati Washington ikiongeza shinikizo dhidi ya Tehran na makundi yanayoungwa mkono na Iran.
Wizara ya fedha ya Marekani katika taarifa yake imesema iliyalenga makampuni, watu binafsi na meli zinazotuhumiwa kuhusika katika usafirishaji wa bidhaa za Iran, ikiwemo mafuta na gesi ya petroli (LPG) kwenda Yemen na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa niaba ya mtandao wa maafisa wa kifedha wa ki-Houthi.
Imesema mapato kutoka mtandao wa Sa'id al-Jamal yanasaidia kufadhili Wa-houthi wakilenga meli katika bahari ya Shamu na miundombinu ya raia.
Mashambulizi ya meli katika Bahari ya Shamu yanayofanywa na washirika wa wanamgambo wa ki-Houthi yameharibu njia ya meli muhimu kwa biashara ya mashariki hadi magharibi, huku usafirishaji wa mizigo ukishinikizwa kuwa katika viwango vya juu na kusababisha msongamano katika bandari za Asia na Ulaya.