Marekani ikishirikiana na G7 waongeza vikwazo kwa Russia

Chansela wa Ujerumani Angela Merkel (C) akiwa na viongozi wa G7 huko Schloss Elmau, Germany.

Rais wa Marekani Barack Obama na viongozi wa ulaya walikubaliana kuimarisha vikwazo dhidi ya Russia kama haitaanza kutekeleza makubaliano ya Minsk na kuheshimu uhuru wa Ukraine. Mkutano wao ulimalizika Jumatatu baada ya kugusia masuala mbali mbali ikiwemo biashara, mabadiliko ya hali ya hewa na ugaidi.

Bwana Obama alitumaini kuwasilisha ujumbe wa pamoja kwa Russia na alifanikiwa kile alichotarajia baada ya kuwapata wanachama wa ulaya wa G7 kukubali kuongeza muda wa vikwazo ambavyo vinatarajiwa kuisha muda wake katika kipindi cha miezi miwili ijayo jambo ambalo lilikuwa ni changamoto kwa Rais Obama.

Rais wa Marekani, Barack Obama

“Washirika wetu wa ulaya wameunga mkono kwamba wataendeleza vikwazo kwa Russia hadi makubaliano ya Minsk yanatekelezwa kikamilifu, ikimaanisha kuongeza muda wa vikwazo vya EU vilivyokuwa vinaisha muda wake baada ya mwezi Julai”.

Marekani na wanachama wengine wa G7 pia walikuwa na onyo kwa moscow, wanachama katika kundi hilo wapo tayari kuweka vikwazo vya ziada kama Russia haitaanza kuheshimu uhuru wa Ukraine.

Katika matamshi yake mwishoni mwa mkutano wa siku mbili bwana Obama alisema Rais wa Russia, Vladimir Putin anahitajika kufanya maamuzi.

Rais Obama alielezea juhudi zake za kusukuma kupitishwa kwa makubaliano makubwa ya biashara na washirika kote katika Pacific na Atlantic. Na alitoa wito kwa ulaya kusaidia kutatua tatizo la deni la Ugiriki.

Mkutano huo ulijumuisha kikao juu ya ugaidi suala ambalo linaleta wasi wasi mkubwa kwa mataifa ya G7 ambapo baadhi ya mataifa hayo yanashiriki katika mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Marekani kwa wanamgambo wa kundi la Islamic State.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari na David Cameron wa Uingereza

Bara la Afrika lilikuwa na mchango mkuu katika mkutano huo. Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari alikabirishwa kuzungumza kuhusu juhudi za serikali yake dhidi ya kundi la Boko Haram, na Rais wa Liberia, Ellen Johson Sirleaf pia alijiunga katika kujadili mafunzo waliyoyapata katika mlipuko wa karibuni wa Ebola huko Afrika magharibi.

Viongozi wa G7 wana nia ya dhati kuzuia milipuko ijayo kwa kutoa misaada kwa nchi 60 ikiwemo zile za Afrika magharibi.