Marekani, China zakubaliana suala la Korea Kaskazini

Waziri wa Mambo ya Nje Rex Tillerson

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson amesema “hakuna mgogano wowote kati ya Marekani na China juu ya suala la Korea Kaskazini” kufuatia mazungumzo yaliyofanyika Beijing kati ya Rais Donald Trump na Kiongozi wa China Xi Jinping.

Tillerson, ambaye yuko katika mji mkuu wa China pamoja na Trump, alizungumza na waandishi wa habari Alhamisi baada ya viongozi hao wawili kufanya mazungumzo ya pamoja yakiangaza Korea Kaskazini na biashara.

Amesema viongozi hao wawili walikuwa wawazi katika mazungumzo yao juu ya masuala ya haki za binadamu na migogoro ya bahari katika eneo la South China Sea.

Kuhusu Pyongyang, amesema Wachina wameweka wazi na bila ya kupinga katika mazungumzo ya siku mbili kuwa hawatakubali kuwepo Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia.

“Hakuna mwanya wowote katika kufikia malengo ya pande zetu mbili,” amesema Tillerson. “Tunayo maoni yetu juu ya mbinu, muda na kwa kiwango gani tuweke shinikizo na juu ya hilo ndiyo tumetumia muda mwingi katika kubadilishana mawazo.”

Trump kwa mujibu wa Tillerson, amemwambia Xi: “Wewe ni mtu shupavu, naamini unauwezo wa kutatua tatizo hili kwa ajili yangu.”

Kabla ya hapo Rais Trump amesema kuwa Marekani na China ni lazima zifanye kazi pamoja kulikomboa eneo hilo na dunia kwa kile alichokiita ni tishio baya mno linalofanywa na utawala unaofanya mauaji Korea Kaskazini.

Trump aliyasema hayo alipokuwa amesimama na Rais wa China Xi Jinping wakati wakitoa maelezo yaliyokuwa yametayarishwa mmoja baada ya mwengine, lakini hawakutoa fursa ya maswali kutoka kwa waandishi.

Trump ameongeza kuwa Washington na Beijing wamekubaliana kutorudia makosa ya siku za nyuma katika kukabiliana na Pyongyang, ambao kwa miaka kadhaa sasa wameweza kwa haraka kupiga hatua katika programu yao ya silaha za nyuklia na makombora ya balistika.

Trump mapema alisema maendeleo ni mazuri katika mazungumzo yake na Xi.

“Dunia nzima yenye ustaarabu lazima ishirikiane katika kukabiliana na hatari ya Korea Kaskazini,” Trump alisema.

Katika maelezo yake yaliyokuwa yametayarishwa, kauli ya Xi ilikuwa siyo wazi sana juu ya Korea Kaskazini, akisema, “tumesisitiza kuwa na msimamo thabiti katika kuondoa silaha za nyuklia katika rasi hiyo.”

“Naamini kuwa tunasuluhisho kuhusu hilo, kama mlivyokuwa nalo nyinyi,” Trump alimwambia Xi wakati wa mazungumzo marefu ya pamoja Alhamisi asubuhi katika mji mkuu wa China.

Baadae, wakati Trump na Xi wakizungumza katika mkutano wa viongozi wafanyabiashara, Trump alisema, “namshukuru Rais Xi kwa juhudi zake za hivi karibuni kukabiliana na Korea Kaskazini na kusitisha mahusiano yao na taasisi za fedha za Korea Kaskazini.