Jeshi la Sudan na kikosi cha Rapid Support Forces walikubaliana rasmi jana Jumatatu kuongeza kwa siku tano za sitisho la mapigano kwa ajili ya usambazaji wa misaada ya kibinadamu, sitisho hilo limefikiwa chini ya upatinishi wa Marekani na Saudi Arabia, lakini lilikiukwa mara kwa mara wiki iliyopita.
Tangu muda wa kusitisha mapigano kuongezwa, mapigano zaidi yaliripotiwa na wakazi, yakiwemo mapigano kwa kutumia aina mbalimbali za silaha kusini mwa Khartoum, na mapigano katika jimbo la Nyala la Darfur Kusini.
Mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani, kamanda wa kikosi cha RSF Mohammed Hamdan Dagalo, kwa mara nyingine wamelaumiana kukiuka makubaliano hayo na kudai kwamba wamejibu uchokozi wa adui.
Vita hivyo vimeua watu 1,800, na zaidi ya watu milioni 1 wamelazimika kuhama makazi yao na karibu watu 350,000 walikimbilia katika nchi jirani, Umoja wa Mataifa umesema.