Mapigano yamezuka kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23 na kusababisha walinda amani wanane wa Umoja wa Mataifa kujeruhiwa baada ya utulivu wa muda mfupi huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Umoja wa Mataifa umesema.
Mmoja wa walinda amani “alijeruhiwa vibaya” katika shambulio la Jumamosi huko Sake, alisema mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Bintou Keita. Mji huo wa kimkakati uko kilomita 20 magharibi mwa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, na mapigano yameanza tena katika eneo hilo siku ya Jumamosi, walioshuhudia wamesema, baada ya siku kadhaa za utulivu.
Kufikia Jumapili mchana, hali ya utulivu ilirejea katika eneo hilo, mashahidi waliongeza. Chanzo cha usalama cha Congo kimeliambia shirika la habari la AFP kuwa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa walijeruhiwa wakati makombora mawili ya M23 yalipopiga kwenye kambi yao katika wilaya ya Mubambiro huko Sake.