Mapigano ya Israel na Hamas yapamba moto Jumapili

Mapigano makali kati ya Israel, na wanamgambo wa Hamas, yameendelea Jumapili katika mji wa Khan Younis kusini mwa Gaza.

Wapalestina waliambiwa kuondoka kwenda kusini mwa Gaza, ili kuepuka mapigano upande wa kaskazini lakini sasa mapigano yamekwenda hadi kusini.

Watu 9 tu kati ya 10 huko Gaza, wana uhakika wa kula chakula kila siku, kwa mujibu wa Carl Skau, naibu mkurugenzi wa shirika la mpango wa chakula Duniani. Jeshi la Israel linasema mashambulizi yake lazima yasonge mbele na kupanua operesheni zake kusini mwa Ukanda wa Gaza.

“Kifo na maumivu yoyote kwa raia ni jambo baya, lakini kwa sasa hatuna njia mbadala,” Luteni Kanali Richard Hecht, ameliambia shirika la habari la Uingereza BBC, Jumamosi.

Mshauri wa usalama wa taifa Tzachi Hanegbi, amesema Israel imewauwa takriban wanamgambo 7,000 wa Hamas mpaka sasa, lakini hakusema makadirio hayo yamepatikana vipi.