Mapigano kwenye mpaka wa Iran na Pakistan

Rais wa Iran Ebrahim Raisi (Kulia) akiwa katika mkutano na waziri mkuu wa Pakistan Shahbaz Sharif May 18, 2023

Walinzi sita wa mpakani wa Iran wameuawa katika mapambano na kundi lenye silaha lisilojulikana, lililokuwa linajaribu kuingia nchini humo.

Televisheni ya taifa ya Iran imeripoti kwamba makabiliano hayo yametokea karibu na mpaka na Pakistan.

Mapigano yametokea katika mji wa Saravan, katika jimbo la kusini mashariki, la Sistan na Baluchistan, kiasi cha kilomita 1,360 kusini mashariki mwa mji mkuu wa Tehran.

Bila kutoa ufafanuzi zaidi, ripoti imesema kwamba washambuliaji walikimbia kutoka sehemu hiyo wakiwa wamewabeba wenzao waliouawa.

Televisheni ya Iran vile vile imesema kwamba walinzi wa pwani wawili wamejeruhiwa katika tukio hilo.

Hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na shambulizi hilo hadi wakati tunaandaa ripoti hii.

Sehemu ambapo mapambano yametokea ni mojawapo ya sehemu za Iran zisizokuwa na maendeleo na inayokaliwa na wasunni wenye uhusiano mbaya na utawala wa wakishia.