Mashahidi waliko mashariki mwa mji mkuu waliripoti mashambulio ya bunduki, huku wengine waliko katika vitongoji vya kaskazini wakisema mashambulio makali ya mizinga kutoka kambi ya jeshi yalitikisa kuta za nyumba.
Mashambulizi ya angani kwa mara nyingine tena yameathiri maeneo kadhaa ya jiji la Khartoum.
Huko Omdurman, mji pacha na Khartoum ulioko ng'ambo ya pili ya Mto Nile, "mashambulizi makali ya mabomu ya anga na silaha za kushambulia ndege" yaliendelea “kwa zaidi ya saa mawili mfululizo", shahidi mmoja aliliambia shirika la habari la AFP.
Katikati ya mji wa Khartoum, walioshuhudia walisema mapigano yalizuka mitaani huku "ndege za kijeshi zikiruka juu" katika eneo ambalo "lilikuwa shwari kwa siku kumi."
Nchi hiyo ya Sudan inayokumbwa na vita, mji mmoja kwenye mto wa Blue Nile umekuwa mahala watu wanakimbilia ili kuepuka mapigano, lakini waathirika wanaoishi katika mji huo wanavumilia msongamano, magonjwa yanayoenea na njaa inayojitokeza.
Watu wengi wamepata hifadhi katika kambi za muda zilizowekwa katika shule, mabweni ya chuo kikuu na majengo mengine huko Wad Madani, mji uliyoko kwenye ukingo wa Blue Nile katika eneo la kilimo cha pamba katika jimbo la Al-Jazirah.