Mapambano makali yaendelea Syria

Rais wa Syria, Bashar al-Assad

Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Marekani wanashinikiza kuthathmini siku 45 za kazi za waangalizi wa UN nchini Syria

Wanaharakati nchini Syria wanasema mapambano kati ya waasi na majeshi ya serikali katika mji mkuu Damascus yanaendelea kwa siku ya tatu katika kile kinachoonekana kuwa kipindi cha mapigano makali katika mji huo tangu ghasia za kisiasa dhidi ya Rais Bashar al-Assad zianze.

Picha za video zilizowekwa kwenye mtandao Jumanne zilionekana kuonyesha wakazi wa Damascus waliokuwa na khofu wakikimbia mapigano mwanzoni mwa wiki.
Mapigano yametokea wakati baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linajibizana juu ya maazimio mawili ya kukabiliana na Syria.

Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Marekani wanashinikiza kutathmini siku 45 za kazi za waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria pamoja na kitisho cha vikwazo dhidi ya serikali ya Assad. Russia inapendekeza wito wa kuongeza muda wa kazi za Umoja wa mataifa, lakini sio vikwazo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon anaitembelea China huku mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Kofi Annan anafanya mazungumzo na rais wa Russia Vladimir Putin mjini Moscow.

Russia na China awali walitumia kura zao za turufu kupinga maazimio ya baraza la usalama yaliyotaka kuchukua hatua kali dhidi ya Syria.