Katika tangazo ambalo lilikuwa likitarajiwa na baadhi ya wadau, waandalizi wa michezo ya Olimpiki Tokyo 2020, iliyokuwa imepangwa kuanza tarehe 24 Mwezi Julai, walisema kwamba michezo hiyo itaahirishwa kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki lilifikia uamuzi huo baada ya kujadili suala hilo kwa wiki nne.
"Napendekeza tuahirishe michezo hii kwa mwaka mmoja, Rais wa [IOC] Thomas Bach kwa 100%," alisema Abe.
Wachezaji binafsi, timu mbalimbali za michezo duniani kote na wadau wengine walikuwa na maoni mseto huku baadhi wakielezea kuhuzunishwa kwao na wakati huo huo, wakieleza kwamba kulikuwa na umuhimu wa kuchukua hatua hiyo.
"Michezo silo jambo muhimu zaidi kwa sasa. Lililo muhimu ni kuokoa maisha," alisema rais wa kamati ya michezo ya olimpiki kwa walemavu, Andrew Parsons.
Andy Anderson, Afisa mkuu wa chama cha Olimpiki nchini Uingereza alisema amesikitishwa mno na hatua hiyo, lakini akaongeza kwamba ilikuwa muhimu kuahirisha michezo hiyo.
Gumzo lilikuwa linaendelea kwa muda kuhusu uwezekano wa kuahirishwa kwa michezo hiyo ambayo ina umaarufu mkubwa mno, na ambayo uandaaji wake hugharimu kiasi kikubwa cha pesa, kuziletea taadhima nchi zinazoshiriki na kuleta faida kubwa kwa wafanyabiashara.
Katika taarifa ya pamoja siku ya Jumanne, waandalizi wa Tokyo 2020 na IOC walisema:
"Kutokana na kasi ya mlipuko wa wa coronavirus hali kuwa mbaya duniani kote...bodi ya utendaji leo imeanzisha mchakato mpya wa mpango wa mazingira maalum."
Hii ni mara ya kwanza kwa michezo hiyo kuahirishwa tangu mwaka wa 1944.