Mamilioni kukabiliwa na njaa, Sahel

Picha ya wanajeshi wakiwa kwenye jangwa la Sahara

Umoja wa Mataifa umeonya kwamba takriban watu milioni 18 kwenye eneo la kaskazini mwa Afrika la Sahel huenda wakakabiliwa na baa la njaa katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.

Hali hiyo inasemekaa ni kutokana na athari za vita vya Russia nchini Ukraine, janga la corona, mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na kupanda kwa gharama ya maisha. Taarifa kutoka kwenye ofisi ya kuratibu masuala ya kibinadamu ya Umoja huo imesema Ijumaa kwamba hali hiyo huenda ikasababisha watu wengi kuhama kutoka kwenye maeneo yaliyoathiriwa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, watu wengi wamekuwa wakikabiliana na njaa tangu mwaka 2014 wengi wao wakitokea Burkina Faso, Chad, Mali na Niger wakati milioni 1.7 miongoni mwao wakihitaji misaada ya dharura ya chakula kulingana na Umoja wa Mataifa. Wakazi wengi wa eneo la Sahel lililoko kusini mwa jangwa la Sahara ni wahamiaji wanaolenga kuingia barani Ulaya kwa matumaini ya kujikwamua kiuchumi, wakati pia wakitafuta usalama wao.