Mamia ya safari za ndege zasitishwa kutokana na corona

Ndege zikiwa kwenye uwanja wa ndege wa Boston hapa Marekani

Mashirika kadhaa ya ndege hapa Marekani yamesitisha mamia ya safari za ndege kwa siku tatu mfululizo kufikia Jumapili.

Hatua hiyo ni kutokana na kuongezeka kwa virusi vipya vya corona vya omicron wakati maelfu ya watu wakilazimika kutosafiri kwa ajili ya sherehe za sikukuu,huku mamia ya wafanyakazi wa ndege hizo pia wakibaki nyumbani.

Safari za ndege takriban 650 zilifutwa Jumapili kuingia na kutoka nchini 1,000 zikipunguzwa siku ya Chrismasi huku nyungine 700 zikisitishwa wakati wa mkesha wa krismasi kwa mujibu wa mtandao unaofuatilia safari za ndege wa FlightAware.com.

Inatarajiwa kwamba safari zaidi za ndege zitasitishwa katika siku zijazo. Taarifa zinaongeza kusema kwamba karibu safari 2,150 za ndege zimesitishwa Jumapili kote ulimwenguni wakati nyingine 5,798 zikicheleweshwa.

Virusi vya Omicron viligundulika kwa mara ya kwanza mwezi Novemba nchini Afrika kusini wakati sasa hivi vikisemekana kuchangia takriban robo tatu ya jumla ya maambukizi yote hapa Marekani. Kulingana na takwimu zilizofuatiliwa na shirika la habari la Reuters, idadi ya maambukizi mapya hapa Marekani imepanda kwa asilimia 45 katika wiki moja iliyopita.