Serikali ya Mali ambayo imebanwa kutokana na vikwazo vilivyochukuliwa na Jumuia ya nchi za Afrika magharibi (ECOWAS), imeshindwa kulipa madeni yake kwenye soko la fedha la kanda hiyo tangu mwishoni mwa mwezi Januari, imesema taasisi inayosimamia shughuli za kifedha na kiuchumi kwenye jumuia hiyo.
Tangu tarehe 31 Januari taasisi hiyo ilichapisha taarifa tano kwa wawekezaji ikieleza kwamba Mali ilishindwa kutekeleza wajibu wake wa kulipa madeni.
Kiwango cha madeni ambayo hajalipwa ni sawa na euro milioni 81.
Taasisi hiyo ilisema katika taarifa yake ya hivi karibuni kwamba “ hali hiyo ya kushindwa kulipa madeni inajiri wakati serikali ya Mali iko chini ya vikwazo vilivyochukuliwa na nchi wanachama wa ECOWAS.
Taasisi hiyo ya kifedha na kiuchumi inajumuisha nchi nane za Afrika magharibi zinazotumia sarafu ya CFA, ambazo ni Ivory Coast, Senegal, Togo, Burkina Faso, Mali, Guinea Bissau, Niger na Benin.