Mali inaomba wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kuondoka nchini humo mara moja

Wanajeshi wa Senegal wa Kikosi cha Umoja wa mataifa nchini Mali (MINUSMA), Julai 24, 2019.

Waziri wa mambo ya nje wa Mali Abdoulaye Diop, Ijumaa aliomba walinda amani wa Umoja wa Mataifa kuondoka mara moja nchini humo.

Diop aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba Mali inataka kikosi cha ulinzi wa amani cha Umoja wa Mataifa( MINUSMA) nchini Mali, “kiondolewe bila kuchelewa.”

“Minusma inaonekana kuwa sehemu ya matatizo kwa kuchochea mivutano kati ya jamii yanayozidishwa na madai makubwa ambayo yanahatarisha sana amani, maridhiano na mshikamano wa kitaifa nchini Mali,” waziri huyo alisema.

Diop aliliambia Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa “Hali hii inasababisha kutoaminiana kati ya wananchi wa Mali na kusababisha pia mzozo wa imani kati ya viongozi wa Mali na MINUSMA.”

Taifa hilo la Afrika Magharibi linakabiliwa na uasi tangu mwaka 2012. Kikosi cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kilipelekwa nchini humo mwaka 2013 lakini hali ya ukosefu wa usalama inaendelea.