Maelfu ya watu Jumatano walikumbana na baridi kali ili kwenda katika jengo la Bunge la Marekani, ili kutoa heshima zao za mwisho kwa rais wa zamani Jimmy Carter, amabye mwili wake umelazwa katika jengo hilo kabla ya mazishi yake ya kiserikali ya kifahari kufanyika Alhamisi.
Waombolezaji ambao walijumuisha maafisa kadhaa waliochaguliwa pamoja na makamu wa rais Kamala Harris, waliangazia baadhi ya mafanikio yake na ubinadamu wa kiongozi huyo aliyefariki mwezi uliopita akiwa na umri wa miaka 100.
David Smith profesa kwenye chuo cha Carter cha Amani na Usuluhishi wa Mizozo kwenye chuo kikuu cha George Mason, alisema kuwa rais huyo wa zamani alikuwa na ushawishi mkubwa kwenye maisha yake, wakati akiambia VOA kwamba alifika Bungeni, ili kutoa heshima zake mwisho kwa Carter pamoja na miradi aliyobuni.