White House na bunge la Marekani walionekana kufikia makubaliano Jumatano ya mpango wa matumizi ili kuepuka kufungwa kwa baadhi ya operesheni za serikali kuu Ijumaa usiku lakini makubaliano hayajumuishi dola bilioni tano ambazo Rais Donald Trump alizitaka kwa ajili ya ujenzi wa ukuta kwenye mpaka wa Marekani na Mexico.
Kiongozi wa baraza la seneti m-Republican Mitch McConnell alisema baraza hilo litapiga kura baadae juu ya kiwango cha fedha kwa ajili ya operesheni za robo mwaka kwa serikali kuu ya Marekani hadi Februari 8 wakati Rais Trump na wabunge kwa mara nyingine watakapokabiliana na uwezekano wa kufungwa kwa baadhi ya operesheni katika serikali kuu.
Kiongozi wa Democrat Charles Schumer alisema wa-Democrat wataunga mkono mpango wa matumizi wa muda mfupi pamoja na sehemu ya serikali ya Marekani ambayo tayari imeshapata bajeti hadi mwishoni mwa Septemba mwaka ujao.
Rais Trump aliahidi wakati wa kampeni yake mwaka 2016 kujenga ukuta kwenye mpaka wa Marekani na Mexico ili kuzuia wahamiaji haramu kuingia na kwamba Mexico italipia gharama za ujenzi huo.