Makubaliano ya sitisho la mapigano kati ya Israel na Hamas yaanza kutekelezwa, pande zote kuachilia huru mateka

Magari ya kijeshi ya Israel yaonekana karibu na mpaka wa Israel baada ya kuondoka Gaza, kufuatia makubaliano ya sitisho la muda la mapigano kati ya Hamas na Israel, Novemba 24, 2023.

Makubaliano ya sitisho la mapigano kwa siku nne kati ya Israel na Hamas yameanza kutekelezwa Ijumaa saa moja asubuhi majira ya huko, yakitarajiwa kufuatiwa na kuachiliwa huru kwa zaidi ya mateka 10 wanaoshikiliwa na Hamas na Wapalestina 150 wanaoshikiliwa na Israel.

Makubaliano hayo yanajumuisha usitishwaji kamili wa mapigano kaskazini na kusini mwa Gaza, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar Majed Al-Ansari aliwaambia waandishi wa habari mjini Doha.

Kulingana na makubaliano hayo, wanawake 50 na watoto waliotekwa nyara na Hamas tarehe 7 Oktoba wataachiliwa huru kwa mabadilishano ya Wapalestina 150 wanawake na watoto walio jela nchini Israel.

Mateka 13 wataachiliwa huru leo Ijumaa kutoka Gaza, na makundi mengine ya mateka wataachiliwa huru kila siku hadi mateka wote 50 waachiliwe huru.

“Sote tunatarajia kwamba makubaliano haya yatatoa fursa ya kuanza kazi pana ya kufikia sitisho la kudumu la mapigano,” Al-Ansari alisema.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Israel inatakiwa kusitisha mashambulizi yake huko Gaza kwa siku nne, kadhalika, Hamas ilithibitisha kwenye mtandao wake wa Instagram kwamba mashambulizi ya wapiganaji wake yatasitishwa pia.