Kampuni kubwa binafsi ya kuzalisha umeme DTEK, imesema kwamba makombora ya Russia yamesababisha uharibifu mkubwa kwa mitambo yake mitatu kati ya sita nchini Ukraine.
Gavana wa Lviv Maksym Kozytskyi, ameandika ujumbe wa Telegram kwamba makombora ya Russia yameharibu vituo vya kuzalisha umeme katika wilaya ya Chervonohrad na katika wilya ya Stryi.
Hakuna ripoti za vifo.
Kwingineko Gavana wa Korovohrad ameripoti kifo cha mtu mmoja na 13 kujeruhiwa, pamoja na nyumba kadhaa kuharibiwa katika mashambulizi ya Russia.
Maafisa katika Vinnytsia vile vile wameripoti mashambulizi ya makombora ya Russia ambayo yameharibu miundo mbinu muhimu.
Jeshi la anga la Ukraine limesema kwamba mfumo wake wa ulinzi umeharibu makombora 39 kati ya 55 yaliyorushwa, na ndege zisizokuwa na rubani 20 kati ya 21.