Makamu Rais wa Marekani, Joe Biden, alisema kuwa utekelezaji wa mauaji ya watu wengi uliotokea mjini Orlando katika jimbo la Florida nchini Marekani sasa umeanza kueleweka, huku wachunguzi wakijaribu kutathmini kilichopelekea shambulio hilo lililowaacha watu 49 kufariki na 53 kujeruhiwa.
Biden hakufafanua zaidi lakini akasema kuwa katika siku za hivi karibuni, Rais Barack Obama atalizungumzia swala hilo kwa kina. Obama anatarajiwa kuzuru mji wa Orlando siku ya Alhamisi.
Kwa maneno yake mwenyewe, Rais Obama alisema siku ya Jumanne kuwa shambulizi hilo lilitekelezwa na kijana aliyekuwa na hasira, aliyetatizika kiakili na ambaye alijifunza itikadi kali.
Alisema hakukuwa na ushahidi wowote kuwa kundi lolote la kigaidi kutoka nchi za nje lilimwelekeza Omar Mateen, mwenye umri wa miaka 29, kutekeleza shambulizi hilo lililofanyika kwenye klabu moja ya mashoga.