Jeshi la Ukraine lilisema limetungua jumla ya droni 26 zilizorushwa na Russia.
Maafisa huko Kyiv walisema mabaki ya ndege hizo yaliyoanguka baada ya kutunguliwa yaliharibu majengo kadhaa ya makazi ya raia.
Huko Odesa, gavana wa mkoa Oleg Kiper alisema droni mbili zilipiga majengo ya utawala katika bandari hiyo, wakati mabaki ya droni zilizotunguliwa zilisababisha kituo cha kuhifadhi nafaka na kituo kingine kushika moto.
Odesa ni bandari kuu iliyohusika na juhudi za nafaka katika bahari ya Black Sea, makubaliano yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki ambayo yaliruhusu kuanza tena usafirishaji muhimu wa nafaka kutoka bandari za Ukraine ambazo zilikuwa zimedhibitiwa na uvamizi wa Russia nchini Ukraine.
Mpango huo ni pamoja na usafirishaji nje wa mbolea na chakula cha Russia. Russia imelalamika kuwa sehemu ya makubaliano haijatekelezwa na imesema hakuna sababu ya kuongeza muda wa mkataba huo zaidi ya Julai 17 unapomalizika.
Umoja wa Mataifa ulisema Jumatatu kuwa zaidi ya tani za metriki milioni 32 za bidhaa za chakula zimesafirishwa kupitia bandari tatu za Ukraine tangu juhudi za usafirishaji huo zilipoanza Agosti 2022.
Umoja wa Mataifa ulisema kuwa usafirishaji huo wa nafaka ulikwenda katika nchi 45, ikiwemo ngano iliyosafirishwa na Shirika la Chakula Duniani (WFP) kwenda kwa watu wenye shida huko Afghanistan, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan na Yemen.
Chanzo cha habari hii ni mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters.