Mahakama yatoa onyo kwa madaktari Tanzania

  • Sunday Shomari

Wagonjwa wakihamishwa kwa kukosa huduma ya madaktari Muhimbili.

Athari kutokana na mgomo wa madaktari nchini Tanzania sasa zimeanza kudhihirika wazi.

Mahakama kuu ya Tanzania Kitengo cha kazi kimetoa onyo kwa Chama cha Madaktari Nchini (MAT) kuzingatia amri ya Mahakama hiyo iliyotolewa siku ya Ijumaa tarehe 22 Juni 2012 ya kusitisha na kutoshiriki katika mgomo na kumtaka Rais wa Chama cha Madaktari kutangaza kutii amri hiyo kupitia vyombo vya habari.

Athari kutokana na mgomo wa madaktari nchini Tanzania sasa zimeanza kudhihirika wazi, kufuatia kusimama kwa huduma katika baadhi ya hospitali huku baadhi ya wagonjwa wakianza kurejea makwao wakiwa katika hali ya kukata tamaa.

Hata hivyo hadi sasa bado serikali haijatoa tamko lolote kutokana na hali hiyo, huku madaktari wakiendelea kusisitiza kuendelea na mgomo huo mpaka kutakapopatikana suluhu ya kudumu.

Mwandishi wetu George Njogopa anaarifu kuwa wagonjwa wamekuwa wako katika hali ya kukata tamaa na serikali haina jibu , madaktari wamesisitza hawako tayari kurudi kazini mpaka waboreshewe mazingira ya kufanya kazi, kuongezewa kwa kima cha chini cha mshahara na kuwepo kwa marupu rupu ya kazi.

Na mahakama kuu nchini humo Jumanne ilitoa tamko la kusisitiza madaktari hao kurudi kazini mbele ya Naibu mwanasheria mkuu George Masadi na Rais wa chama cha Madaktari Tanzania kuwa madaktari hao warudi kazini au watachukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza na Sauti ya Amerika, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini Tanzania Dk.Steve Ulimboka alikana kupokea taarifa yeyote ya kusitisha mgomo wao kutoka mahakama kuu akieleza kwamba hajapokea barua yeyote. Pia aliongeza kwamba wao hawana uhusiano wowote na chama cha madaktari Tanzania (MAT) na kwamba wao wanaweza kudai haki zao kwa njia yeyote.

Mgomo huo ulitokea miezi minne iliyopita nchini humo na bado upande wa madaktari ni kitendawili kama watarudi kazini au la baada ya waziri wa afya nchini humo kuwataka madaktari hao kurejea kazini na wito huo kurejelewa Jumanne na mahakama kuu ya Tanzania.