Amri hiyo ya Mahakama ya Kimataifa ya sheria mjini the Hague, ambayo inaiwajibisha Israeli kisheria, iliitaka nchi hiyo kuchukua “ hatua zote zinazohitajika na zenye ufanisi kuhakikisha bila kupoteza muda” kwamba huduma za msingi na msaada wa kibinadamu unapelekwa huko,” ikiwemo chakula, maji, mafuta na vifaa vya matibabu.
Mahakama hiyo iliamuru pia Israel kuhakikisha mara moja “kwamba jeshi lake halitekelezi tena vitendo ambavyo ni ukiukaji wa haki yoyote ya Wapalestina huko Gaza kama kundi la watu wanaolindwa chini ya mkataba kuhusu kuzuia na kuadhibu uhalifu wa mauaji ya kimbari, ikiwemo kuzuia, kupitia hatua yoyote, utoaji wa msaada wa dharura wa kibinadamu.”
Mahakama imeiomba Israel kutoa ripoti ndani ya mwezi mmoja kuhusu jinsi ilivyotekeleza amri hizo.
Israel haikutoa mara moja maelezo juu ya uamuzi huo, lakini ilikanusha vikali kufanya mauaji ya kimbari katika mwenendo wake katika vita vya karibu miezi sita dhidi ya wanamgambo wa Hamas. Iliitaka Mahakama hiyo ya Umoja wa mataifa kutotoa amri mpya.