Mahakama ya juu ya Marekani yabatilisha sheria za New York zinazopiga marufuku kubeba bunduki hadharani

Mahakama ya juu ya Marekani, picha ya AP

Meya wa jiji la New York na gavana wa jimbo la New York Alhamisi wamelezea hofu kubwa baada ya mahakama ya juu ya Marekani kubatilisha sheria kali zilizochukuliwa na jimbo hilo kuhusu kubeba bunduki hadharani, wakisema watu wengi zaidi watakuwa wanatumia bunduki kiholela.

Meya Eric Adams, mdemocrat na mkuu wa zamani wa polisi, ametabiri kwamba malumbano zaidi yatageuka ghasia mara tu itakapokuwa rahisi kubeba bunduki ndani ya mji wa New York wenye zaidi ya wakazi milioni 8, ukiwa mji wenye watu wengi zaidi hapa Marekani.

“Uamuzi huu umefanya kila mmoja wetu asiwe salama kutokana na ghasia za bunduki,” Adams amesema katika mkutano wa waandishi wa habari kwenye makao makuu ya mji wa New York.

Kufikia mwezi huu wa Juni, watu 693 wameuawa kwa kupigwa risasi katika jiji la New York, kulingana na takwimu rasmi, ikilinganishwa na watu 765 waliouawa kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Mahakama ya juu kwa mara ya kwanza iliamua kwamba kifungu cha pili cha katiba ya Marekani, ambacho kinalinda haki ya kumiliki na kubeba bunduki na kuidhinishwa mwaka wa 1791, kinalinda haki ya kila mtu kubeba silaha hadharani ili kujihami.