Mahakama nchini India imeongeza muda wa kushikiliwa kwa kiongozi wa upinzani na waziri kiongozi wa Delhi, Arvind Kejriwal hadi Aprili mosi mwaka huu katika kesi ya rushwa inayohusiana na sera ya pombe ya mji mkuu wa nchi hiyo, vyombo vya habari vya eneo hilo vimesema.
Idara ya kupambana na uhalifu wa kifedha nchini India ilimkamata Kejriwal wiki iliyopita kuhusiana na madai ya rushwa yanayohusiana na sera ya pombe ya mji huo, na alirudishwa rumande hadi Alhamisi, wiki kadhaa kabla ya India kuanza upigaji kura katika uchaguzi mkuu Aprili 19.
Chama cha Kejriwal cha Aam Aadmi Party (AAP) kinasema kesi hiyo imetungwa na ina ushawishi wa kisiasa. Serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi na chama chake cha Bharatiya Janata wamekanusha kuingilia kati kisiasa na kusema mashirika ya kutekeleza sheria yanafanya kazi yao.
Viongozi wote wakuu wa AAP walikuwa tayari kizuizini katika kesi hiyo kabla ya Kejriwal kukamatwa.