Mahakama nchini Kenya yaongeza muda wa amri ya kuizuia serikali kupeleka mamia ya afisa wa polisi nchini Haiti

Polisi wa kukabiliana na ghasia wakati wa maandamano dhidi ya serikali katika mtaa wa Kibera mjini Nairobi, Julai 19, 2023

Mahakama ya Kenya Jumanne imeongeza muda wa amri ya kuizuia serikali kupeleka mamia ya maafisa wa Polisi nchini Haiti katika operesheni inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kwa lengo la kuleta amani katika taifa hilo la Caribbean lililokumbwa na machafuko.

Uamuzi huo unatolewa baada ya Umoja wa Mataifa kuonya kuwa usalama nchini Haiti, ambako magenge ya uhalifu yanadhibiti eneo kubwa la nchi, umezidi kudorora, huku mauaji yakifikia viwango vya juu sana.

Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa mapema mwezi Oktoba lilipitisha azimio la kuruhusu upelekaji wa kikosi cha kimataifa kinachoongozwa na Kenya ili kuwasaidia Polisi wa Haiti.

Lakini Mahakama kuu ya Nairobi baadaye ilitoa uamuzi wa muda katika kesi iliyowasilishwa na mwanasiasa wa upinzani Ekuru Aukot, ambaye alidai kupeleka polisi wa Kenya huko ni kinyume cha katiba kwa sababu hatua hiyo haikuungwa mkono na sheria wala mkataba wowote.