Mahakama Kuu ya Marekani kuamua hatima ya wahamiaji wasio na stakabadhi

IWanaharakati wa uhamiaji wakiandamana mbele ya mahakama kuu mjini Washington wakiunga mkono amri ya kiutendaji ya Rais Barack Obama kuwapatia msamaha wahamiaji haramu.

Mahakama kuu ya Marekani leo inatathmini hatima ya takriban wahamiaji milioni 4 wakati majaji wanaposikiliza hoja za ufunguzi kwa kesi ya kihistoria inayopinga amri ya kiutendaji ya Rais Barack Obama kuhusu uhamiaji.

Uamuzi wa mahakama hiyo utaathiri pakubwa amri za kiutendaji katika siku zijazo na unakuja wakati swala la uhamiaji linazungumziwa sana kwenye kampeni za mwaka huu.

Kesi hiyo maarufu US vs. TEXAS imeiomba mahakama kutathmini iwapo Rais alivuka mamlaka yake ya kikatiba wakati alipotoa amri ya kutowarudisha makwao wahamiaji wasio na stakabadhi.

Uamuzi wa kesi hiyo utaathiri maamuzi kwenye majimbo mengine 25 yanayopinga amri ya rais kuhusu uhamiaji.