Magufuli amfukuza kazi mkuu wa kupambana na rushwa

Rais John Magufuli wa Tanzania

Rais John Magufuli wa Tanzania amemfukuza kazi mkurugenzi mkuu wa taasisi ya kupambana na rushwa (TAKUKURU) nchini humo, Edward Hosea, akisema haridhishwi na jinsi taasisi hiyo inavyofanya kazi zake.

Uamuzi huo ulitangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi wa Ikulu ya Dar es salaam, Balozi Ombeni Sefue, ambaye aliongeza kuwa Rais Magufuli wakati huo huo amemteua aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Valentino Mlolola kuwa kaimu Mkurugenzi Mkuu.

Katika taarifa hiyo Balozi Sefue alisema Rais Magufuli hakupendekezwa na kwamba ingawa taasisi hiyo imekuwepo nchini kwa miaka mingi lakini kumekuwa kukitokea vitendo vya rushwa, hasa upotevu mkubwa wa mapato ya serikali katika mamlaka ya bandari nchini Tanzania.

Rais pia amewasimamisha kazi watumishi waandamizi wa TAKUKURU kwa kuvunja amri ya rais ya kutosafiri nje ya nchi bila kibali cha ikulu. Watumishi hao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas. Mara tu baada ya kuchukua madaraka mwanzoni mwa mwezi Novemba Rais Magufuli alipiga marufuku safari za nje ya nchi kwa maafisa wa serikali ila tu kwa kibali maalum kutoka ikulu.