Magufuli aomboleza kifo cha Kingunge Ngombale Mwiru

Marehemu Kingunge Ngombale Mwiru

Taifa la Tanzania limempoteza mwanasiasa mkongwe Mzee Kingunge Ngombale Mwiru kilichotokea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam mapema leo Ijumaa, taarifa ya Ikulu yaeleza.

Mzee Kingunge Ngombale Mwiru alikuwa akipatiwa matibabu hospitalini hapo baada ya kushambuliwa na mbwa wake nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam Desemba 22, 2017.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais imemnukuu Rais Magufuli akisema taifa limempoteza mtu muhimu.

Marehemu alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kupigania uhuru na baada ya kupata uhuru akiwa mtumishi mtiifu wa Chama cha TANU na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM), na katika nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani ya Serikali.

“Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ametoa mchango mkubwa sana, sisi kama Taifa hatuwezi kusahau na tutayaenzi mema yote aliyoyafanya wakati wa utumishi wake uliotukuka."

Pia rais amesema ametuachia somo la kupigania maslahi ya nchi wakati wote, kuwa wazalendo wa kweli, kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuwa na nidhamu.