Magonjwa yasiyoambukiza kama vile magonjwa ya mshtuko wa moyo, saratani na kisukari yanachangia kwa asilimia 74 ya vifo ulimwenguni na kukabiliana na sababu hatarishi za magonjwa hayo kunaweza kuokoa maisha ya mamilioni ya watu, shirika la afya duniani WHO limesema Jumatano.
Ripoti ya WHO, inasema magonjwa hayo ambayo mara nyingi yanaweza kuzuilika na ambayo yanasababishwa na namna watu wanavyoishi, yanaua watu milioni 41 kila mwaka, wakiwemo watu milioni 17 walio na umri wa chini ya miaka 70.
Maradhi ya moyo, saratani na magonjwa ya kupumua kwa sasa yanazidi magonjwa ya kuambukiza na kuwa magonjwa yanayoua watu wengi zaidi ulimwenguni, imesema ripoti hiyo ya WHO.
“Kila baada ya sekonda mbili, mtu aliye na umri wa chini ya miaka 70 anakufa kutokana na magonjwa yasiyoambukiza, ” Bente Mikkelsen, mkuu wa kitengo cha WHO kinachosimamiya magonjwa hayo, amewambia waandishi wa habari mjini Geneva.
Magonjwa hayo hayasababishi tu vifo vingi duniani bali ripoti inasema yanakua na athari kubwa kwa namna watu wanavyokabiliana na magonjwa ya kuambukiza kama Covid 19 wakiwa na moja kati ya magonjwa hayo.