Mafuriko yauwa watu Sudan Kusini

Mafuriko ya awali Sudan Kusini

Mamlaka ya jimbo la Sudan kusini la Unity imesema kuwa takriban watu 7 wamekufa baada ya mafuriko kusomba nyumba zao kwenye eneo la Mayendit huku familia takriban 400 zikilazimika kuhama makwao katika siku za karibuni.  

Mkuu wa kaunti ya Mayendit, Gatluak Nyang Jumatatu ameambia VOA kipindi cha South Sudan in Focus, kwamba mvua kubwa zimeendelea kunyesha katika wiki kadhaa zilizopita. Watu hao 7 wanasemekana kufa maji kutokana na mafuriko huko wengine 17 wakisemekana kuumwa na nyoka,Nyang ameonegeza kusema.

Amesema pia kwamba takriban asilimia 90 ya ardhi ya Mayendit imefunikwa na maji ambayo pia yameuwa zaidi ya ng'ombe 500 na mbuzi 300. Nyang anasema kuwa watu wengi wanateseka kutokana na magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa mazingira safi, pamoja na malaria kutokana na kuwa hawana neti za kujikinga na mbu.

Mashirika ya kimataifa ya kutoa misaada yameombwa kuingilia kati na kupeleka misaada muhimu ya kibinadamu.