Mafuriko : Watoto wanne waokolewa pangoni Thailand

Watoto wakiangalia picha kabla ya ndugu na rafiki kuanza kufanya maombi maalum kwa ajili ya watoto 12 wa kiumbe na kocha wao waliokwama katika pango lililokumbwa na mafuriko. Watu hao wamekusanyika katika kanisa la Mesai Grace, jimbo la kaskazini mwa Chiang Rai, Thailand, July 8, 2018.

Watoto wa kiume wanne wameokolewa kutoka katika pango lililokuwa limejaa maji huko kaskazini mwa Thailand, mkuu wa kikosi cha uokoaji amesema Jumapili.

Watoto hao wanne walikuwa wamekwama chini ya ardhi pamoja na vijana wengine wanane, walio na umri kati ya miaka 11-16, na kocha wao wa mpira wa miguu mwenye umri wa miaka 25 kwa zaidi ya wiki mbili.

Waokoaji walianza operesheni hiyo ya kuwaokoa vijana hao na kocha wao Jumapili asubuhi. Muda mchache baada ya kiza kuingia, katika majira ya eneo hilo, Jeshi maalum la majini la Thai liliripoti katika ukurasa wake wa Facebook kuwa wanne hao walikuwa wameokolewa.

Mkuu wa operesheni hiyo, Narongsak Osatanakorn, mapema aliwaeleza waandishi kuwa "Leo ndiyo siku ya operesheni maalum."

Maji kutokana na mvua kubwa yamefurika pangoni, na kusababisha timu ya watoto hao kukwama pangoni. Mvua zaidi zinatarajiwa katika wiki zijazo.

Usiku wa Jumapili wazamiaji waliwatoa watoto hao wanne, ambao walikuwa wamevalishwa zana maalum za kuwasaidia kupumua.

Wazamiaji wengine walikuwa wamekaa tayari katika eneo la mwanzoni la kilomita moja ya lango kuu la pango hilo.

Katika baadhi ya maeneo ndani ya pango, watoto hao ilibidi wabebwe ndani ya maeneo yenye mafuriko, baadhi yake yakiwa na upana finyu mno wa meter 0.6.

Operesheni hiyo ya uokoaji ilisababisha kifo cha mmoja wa wazamiaji wa Jeshi la majini la Thai wiki iliyopita.