Waandamanaji waliimba nyimbo zinazoipinga Ufaransa mtawala wa zamani wa kikoloni na Jumuia ya nchi za Afrika magharibi (ECOWAS), ambayo inafikiria uwezekano wa operesheni ya kijeshi ili kumrejesha madarakani rais aliyechaguliwa Mohamed Bazoum ikiwa mashauriano yanayoendelea na viongozi wa mapinduzi yatakwama.
Viongozi wa mapinduzi walipiga marufuku rasmi maandamano lakini kiutendaji, wale wanaounga mkono mapinduzi wanaruhusiwa kuandamana.
Waandamanaji walikuwa na mabango yaliyoandikwa “Sitisha uingiliaji kati wa kijeshi” na “tunapinga vikwazo” wakimaanisha vikwazo vya kiuchumi na biashara vilivyowekwa na Jumuia ya uchumi ya nchi za Afrika magharibi (ECOWAS) siku nne baada ya mapinduzi ya Julai 26.
Maandamano ya Jumapili yaliambatana na wanamuziki kuupongeza utawala mpya wa kijeshi, waandishi wa habari wa AFP wameripoti.
Maandamano hayo ya kuunga mkono mapinduzi yamefanyika siku moja baada ya kiongozi mpya wa kijeshi kuonya kwamba shambulio dhidi ya Niger haitakuwa jambo rahisi kama vile “kutembea ndani ya mbuga”.
Jenerali Abdourahamane Tiani alisema pia katika hotuba kwa njia ya televisheni siku ya Jumamosi kwamba hana azma ya “kunyakua” madaraka na utawala wa mpito kurejesha utawala wa kiraia hautavuka zaidi ya miaka mitatu.