Takribani watu elfu tano walikusanyika katika maandamano hayo, wakipeperusha mabango yanayosema “Sisi ni binadamu, sisi siyo wanyama” na “Plateau lazima iwe huru” kulingana na mwandishi wa shirika la habari la AFP.
Wengi wa waandamanahi hao wakiwa wamevaa nguo nyeusi zikiashiria kuwa wanaomboleza, kundi hilo kubwa lilikusanyika nje ya ofisi ya Gavana wa eneo hilo la mji mkuu wa jimbo la Plateau wakitoa wito wa amani.
Plateau inaligawanya eneo la Kaskazini mwa Nigeria lenye Waislam wengi na eneo la Kusini lenye Wakristo wengi. Mara nyingi linakabiliwa na ghasia za kikabila na kidini.
“Tunatoa wito wa wazi na tunasisitiza kusitishwa kwa mashambulizi yanayoendelea na mauaji hapa Plateau na Nigeria” muandaaji wa maandamano hayo mchungaji Stephen Baba Panya alisema katika hotuba.
“Maafisa usalama wapelekwe katika maeneo yote yenye mashaka ya jimbo la Plateau ili kuzuia mauaji ya Krismas yasirudie”.
Katika shambulio kwenye maeneo ya serikali za mitaa huko Bokkos na Barkin Ladi, yaliyoanza Desemba 23, pale watu wenye silaha walipovamia vijiji na kuwaua watu 198, kulingana na maafisa wa jimbo la Plateau.
Maelfu ya watu walipoteza makazi katika shambulio hilo ambalo liliviathiri zaidi vijiji vya Wakristo.
Chanzo cha Habari hii ni Shirika la habari la AFP