Waandaaji wa maandamano haya ya wanawake yanayofanyika Washington wamesema maelfu ya watu wamehudhuria leo Jumamosi ambayo yanafanyika katika eneo maarufu la National Mall.
Maafisa wa Washington wamesema kuwa mabasi 1800 yamesajiliwa kupaki katika eneo la jiji, ambayo yanaweza kuwa na takriban watu 100,000.
Kadhalika maandamano kama haya yamepangwa pia kufanyika katika miji mikuu 20 dunia nzima, ikiwemo Uiingereza na Sydney.
Madai makuu
Waandaaji wa maadamano wanasema wanataka kutuma ujumbe kwa Trump katika siku yake ya kwanza madarakani kwamba haki za wanawake ni haki za binadamu.
Wanasema kuwa watakuwa pia wanapigia kelele suala la haki za kijinsia na kupinga ubaguzi wa rangi, pia kushinikiza suala la afya na haki za utoaji mimba—vitu ambavyo wanasema viko hatarini kutokana na Trump kuingia madarakani.
Sarah Young, ambaye anashiriki katika maandamano huko Indiana anakoishi ameiambia VOA kwamba kero yake kubwa ni afya ya mwanamke.
“Kuweza kupata ushauri wa uzazi wa majira na kupata matibabu kinamama kumechangia zaidi ya kitu chochote kile katika kumwezesha mwanamke katika karne hii ya 20 na tunakokwenda katika karne ya 21 pia. Iwapo tunataka kuendeleza mafanikio haya, tunahitaji kuwafanyia wepesi wananchi kufikia huduma ya afya,” amesema Young.
Mambo mengine yanayomhamasisha kushiriki maandamano haya ni kushinikiza kukomeshwa kwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, uadilifu wa mazingira, kulinda haki za wafanyakazi, watu wenye ulemavu, wahamiaji na makundi mengine.
Maandamano yanafanyika dunia nzima
Maandamano ya wanawake Washington yatakwenda sambamba na kampeni za maandamano ya wanawake katika miji mikuu mengine ndani ya Marekani na kote duniani, ikiwemo Uingereza na Sydney.
Wakati Lou Ann Homan wa Indiana hatokuwa kati ya wale watakao andamana ambao wamekwenda Washington, ameiambia VOA kuwa yeye atafanya sauti yake isikike pale pale nyumbani anakoishi.
“Kuna vikundi vidogo vidogo vya waandamanaji kote nchini, katika kila mji na jiji, na sisi hapa Indiana , tutakuwa tuko pamoja wengi wetu tukielekea Fort Wayne (Indiana) kuonyesha mshikamano wetu, kuonyesha kwamba tunajali,” amesema.
Harakati hizo za maandamano zimeanza Jumamosi na mkusanyiko mkubwa karibu na bunge la Marekani wakiwemo watumbuizaji na wazungumzaji wakuu, na litafuatiwa mchana na maadamano kutoka eneo la Independence Avenue kwenda ikulu ya White House.
Fikra hii ya maandamano ya wanawake ilianza kwenye Facebook wakati wanawake kote nchini walipokasirishwa na matokeo ya uchaguzi wakaanza kuweka kura za Facebook na kuwahamasisha wenzao kuchukua hatua.
Katika siku chache, baadhi ya hizi kurasa zilikuwa tayari zina wafuasi 10,000 waliojiunga. Wengi wao walieleleza hofu yao kati ya mambo mengine ni juu ya maoni ya Trump kuhusu wanawake.